NEW POSTS

Nape, Zitto watoa hoja muelekeo wa bajeti


Dodoma. Serikali imetakiwa kuepuka kuwa na bajeti ya ‘kisiasa’ badala yake iwe yenye unafuu kwa wananchi wengi ili kuleta maendeleo.

Mbunge wa Jimbo la Mtama (CCM) Nape Nnauye ameyasema hayo leo Juni 14 wakati  akihojiwa na televisheni ya Azam, kuhusu bajeti kuu kwa mwaka wa fedha 2018/19.

Amesema siyo vyema kuwekeza kwenye miradi mikubwa kwa kutegemea fedha za pato la ndani.

“Bajeti ni zaidi ya namba, tunategemea bajeti hii itakuwa na majibu kwa maisha ya watu, tuipe bajeti tafsiri sahihi, natumaini bajeti hii itakuwa na maboresho yenye manufaa kwa wananchi,” amesema Nnauye.

Amesema anaamini kwamba kwa sababu ni bajeti ya kati kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, kuna maboresho mazuri yatakuwa yamefanywa  ili Serikali  ipate nafasi ya kutimiza ahadi zake kwa wananchi.

Kwa upande wake Mbunge wa Kigoma Mjini(ACT-Wazalendo) Zitto Kabwe amesema nchi zilizoendelea   kwa kawaida huwa na fedha wakati zinapotangaza bajeti,  lakini nchi  zinazoendelea hutegemea fedha zitakazokusanywa.

“Katika bajeti ya kwanza tulishindwa kufikia malengo kwa asilimia 14, kwa sababu Serikali ilizidisha bajeti kwa asilimia 31, hivyo ikalazimika kuminya watu ili kufikia lengo, nafikiri makosa haya hayapaswi kurudishwa kwenye bajeti hii,” amesema Kabwe.

Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Dk Bravious Kayonza amesema bajeti ya mwaka wa fedha kwa 2017/18 ilijikita zaidi katika miundombinu badala ya kuwekeza kwa wananchi hasa wa kipato cha chini.

 

No comments