NEW POSTS

‘Housegirl’ atuhumiwa kuiba kichanga cha bosi wake


KAMANDA WA JESHI LA POLISI MKOANI SHINYANGA, SIMON HAULE.

HABIBA Abubakari (20), mkazi wa mtaa na kata ya Nyasubi wilayani Kahama mkoani Shinyanga, anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kumwibia mwajiri wake mtoto mchanga wa bosi wake. 

Habiba ambaye ni mfanyakazi wa ndani anatuhumiwa kuiba mtoto mchanga William Emmanuel, nyumbani kwa bosi alipokuwa akifanya kazi mkoani Singida. 

Tukio la kuibwa kwa mtoto huyo mchanga mwenye umri wa miezi miwili, lilitokea Julai 8, mwaka huu mkoani Singida, ambapo mama wa mtoto huyo, Hawa Rojas (20), alimwacha na Habiba na kwenda kwenye shughuli zake za kibiashara, lakini aliporudi nyumbani hakumkuta mtu yeyote ndipo akawatafuta bila mafanikio. 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Simon Haule, alisema walimkamata Habiba juzi akiwa nyumbani kwao katika mtaa  wake na kata hiyo ya Nyasubi akiwa na mtoto huyo mchanga, ndipo wakamtia nguvuni kisha mtoto kukabidhiwa kwa mama yake mzazi. 

Kamanda Haule alisema taarifa za kuibiwa kwa mtoto huyo walizipata kutoka kwa Jeshi la Polisi mkoani Singida, zikieleza kuwa Habiba anaishi wilayani Kahama, ndipo walipoanza kumsaka na kufanikiwa kumkamata. 

Kwa mujibu wa Kamanda Haule, Habiba atapelekwa Singida kufunguliwa mashtaka kwa kuwa ndipo anapodaiwa kufanya tukio hilo. 

“Baada ya kumhoji alikiri kumuiba mtoto huyo kwa madai kuwa ana tatizo la ugumba lililosababisha kuachana na mumewe (jina tunalihifadhi), ndipo akaamua kufanya hivyo ili kumuonyesha mumewe kuwa hana ugumba kwani ameweza kupata mtoto,” alieleza Kamanda Haule. 

Alitoa wito kwa wazazi kuwa makini na wafanyakazi ambao wanawaajiri kwa ajili ya kuwasaidia kazi za ndani, ikiwamo kufahamu tabia zao, kujua wazazi wao na mahali wanapotoka ili kuepukana na  uwezekano wa watoto wao kuibwa. 

No comments