NEW POSTS

amwomba Magufuli aruhusu mikutano aone nguvu ya upinzani


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Patrick ole Sosopi amesema hatua ya kuzuia shughuli za kisiasa nchini ikiwamo mikutano ya hadhara, imeviongezea vyama vya upinzani uungwaji mkono wa wananchi.

Ili kupima hali hiyo, mwenyekiti huyo ambaye alikuwa akizungumza katika mahojiano maalumu alipotembelea katika ofisi za Mwananchi jijini Dar es Salaam jana, alimtaka Rais John Magufuli kuruhusu mikutano hiyo japo kwa mwezi mmoja, ili kuona nguvu ya upinzani.

Alisema ingawa uamuzi huo umesababisha athari kubwa kwa wapinzani, lakini umeendelea kuwaongezea imani kwa wananchi. “Jambo hili haliathiri Chadema pekee japo sisi tumekuwa champion wa kupinga hali hii, lakini ukweli ni kwamba linaathiri mfumo mzima wa kuwaandaa vijana ili waje kuwa viongozi bora wa baadaye.”

Alisema haiwezekani vyama vya siasa vikaruhusiwa kufanya siasa kipindi cha uchaguzi tu wakati si mahala sahihi pa kuwaandaa vijana.

“Athari kubwa naiona kwa vijana kwa sababu wanapoteza ndoto zao na vipaji vyao; Mfano leo Rais Magufuli ameweza kuongoza kwa sababu marais waliopita waliweka mfumo bora.

“Je, kijana leo akitamani kuwa kiongozi wa siasa atumie njia gani kama hataruhusiwa kuona kwa vitendo namna siasa inavyofanya kazi? Tunaua vipaji vya vijana; lazima tupige kelele,” alisisitiza Ole Sosopi.

Chanzo cha tatizo

“Hofu ilikuwa ni Chadema tungetengeneza populality (umaarufu), hivyo lengo ni kutuficha na kutunyima platform (jukwaa) lakini matokeo yake imekuwa ndivyo sivyo, Watanzania wamefahamu ukweli,” alidai.

Sosopi ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alisema licha ya wapinzani kunyimwa majukwaa ya kufanya siasa, bado chama tawala kimeshindwa kutekeleza ilani na ahadi zake, jambo linalosababisha wananchi kutowaamini.

“Waliahidi kutoa Sh50 milioni kwa kila kijiji wameshindwa kutekeleza kabisa badala yake sasa wanafanya hata yasiyokuwapo katika ilani yao; mfano unawezaje kutoa zaidi ya trilioni moja kwenye mzunguko na kupeleka katika miradi mikubwa kama ya kununua ndege bila ridhaa ya Bunge, huoni kama unatengeneza mgogoro mkubwa? alihoji Ole Sosopi.

Ole Sosopi ambaye mwaka 2015 aligombea ubunge Ismani na kushindwa na William Lukuvi alidai kwa sasa Serikali baada ya kuona imeshindwa, imeamua kufanya mambo yake kwa siri badala ya uwazi kama ilivyokuwa ikijinadi.

“Juzi tumeshuhudia waziri wa sheria na Katiba akisema Serikali imeanza kulipwa na wawekezaji wa madini lakini akasema hilo ni siri. Waziri Mkuu naye amenukuliwa akisema kuwa wataongeza mshahara lakini ni siri, sasa imegeuka kuwa Serikali ya siri,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo wananchi wamejenga imani kubwa kwa Chadema, kiasi kwamba wanaamini kuwa katika uchaguzi mkuu ujao watashinda kwa kishindo.

No comments