NEW POSTS

CCM itashindwa tu ikikataliwa na wananchi, si kwa uimara wa upinzani

Safari ya chama cha upinzani kushinda dola, hupaswa kupitia hatua tano muhimu; mosi, kusajili uwepo wake ili kiruhusiwe kufanya shughuli za kisiasa, pili, kithibitishe uwepo wake, yaani kiwafikie watu na wakione ni hai kivitendo.

Tatu, chama hutakiwa kujijengea utambulisho na kuaminika katika masuala ambayo kinayasimamia. Nne, kujenga matumaini, kwamba wananchi si tu washawishike nacho, bali ndani yake waione kesho yenye matarajio yao.

Tano, chama cha upinzani kina wajibu wa kuwapa sababu wananchi ya kukipigia kura. Kionyeshe kuwa kikipigiwa kura na kushinda, kitakabidhiwa dola.

Hivyo, si iwe ni kuchaguliwa na kushinda kwa hesabu ya kura tu, bali matangazo ya matokeo yamtaje aliye madarakani kuwa ameshindwa.

Kipengele cha tano ni muhimu mno. Nchi za Afrika na maeneo mengi duniani, chama kinaweza kujitosheleza kila eneo lakini kukikosekana uhakika wa chama tawala kukabidhi madaraka baada ya kushindwa, hilo huwa tatizo lenye kukatisha tamaa wapiga kura na hata viongozi wenyewe wa vyama.

Nitatoa mifano miwili ya hivi karibuni zaidi. Mmoja ni Venezuela na mwingine Malaysia. Nchi zote hizo zilifanya uchaguzi Mei mwaka huu. Venezuela Rais aliye madarakani ameshinda, ingawa awali ilionekana amepoteza kukubalika kwake na Malaysia wapinzani wameshinda wakati hawakuwa na nguvu kubwa.

Kwa nini Malaysia ambako upinzani ulionekana kutokuwa na nguvu ndiyo umeshinda? Kilitokea nini mpaka wapinzani Venezuela walioimarika mno mwaka 2015, washindwe kupata ushindi Mei mwaka huu? Majibu yake ndiyo yanabeba mfano kuhusu wapinzani Tanzania na nafasi yao kwenye Uchaguzi Mkuu 2020.

Kilichotokea Venezuela

Desemba 2015, muungano wa vyama vya upinzani Venezuela, unaoitwa Democratic Unity Committee au kwa umaarufu zaidi MUD ulishinda theluthi mbili ya wabunge, wakati chama tawala, United Socialist Party of Venezuela (PSUV) na muungano wao wa Great Patriotic Pole (GPP) ukiambulia theluthi moja.

Kwa mujibu wa taasisi ya utafiti Marekani, Brookings, kupitia taarifa yake iliyoandikwa na Harold Trinkunas Januari 8, mwaka huu, ushindi wa MUD ulimfanya Rais aliye madarakani, Nicolas Maduro apoteze umaarufu.

Brookings waliandika kuwa kila kura za maoni zilipofanyika, Rais Maduro alitajwa chanya kwa asilimia 30 na wananchi wa Venezuela, wakati 70 zikiwa hasi.

Hata mtangulizi wa Maduro, mwasisi wa mapinduzi na Serikali ya Bolivarian, Hugo Chavez kutukuzwa kwake kulipungua hadi kufikia asilimia 30.

Anguko hilo la umaarufu wa Rais Maduro na Serikali ya Bolivarian, lilipata nguvu zaidi kutokana na ongezeko la umaskini kufikia asilimia 81 mwaka 2017, kutoka asilimia 48 mwaka 2014. Idadi ya watoto waliopatwa na utapiamlo ilikuwa kwa kasi na watu wengi walikufa njaa.

Wakati huohuo, familia ya Rais Maduro ikawa inakabiliwa na kashfa kubwa ya dawa za kulevya. Novemba 2015, Flores de Freitas na Campo Flores ambao ni wapwa wa mke wa Rais Maduro, Cilia Flores, walikamatwa Haiti, walipokuwa kwenye harakati za kuingiza dawa za kulevya Marekani.

Kukamatwa kwa wapwa hao wa mke wa rais, kuliipa afya minong’ono kuwa Serikali ya Bolivarian chini ya Maduro na tangu wakati wa Chavez, ilikuwa ikijineemesha kwa biashara ya dawa za kulevya, ikimiliki genge kubwa na lenye nguvu Amerika Kusini. Desemba 2017, vijana hao walihukumiwa kifungo cha miaka 18 jela na Mahakama ya Manhattan, Marekani.

Kimsingi MUD ilikuwa imembana Rais Maduro kila upande na ilitarajiwa mwaka huu PSUV ingekabidhi hatamu ya uongozi kwa muungano huo wa vyama vya upinzani Venezuela. Kinyume chake, Rais Maduro alishinda kwa kishindo kwenye uchaguzi uliofanyika Mei 20, mwaka huu.

Hata hivyo, mwaka 2017 Rais Maduro alicheza mpira mgumu ili kubaki madarakani. Msukumo mkubwa ulitokana na ukweli kwamba endapo angeng’oka kwenye urais, moja kwa moja angefikishwa mahakamani kwa kashfa za rushwa, ufisadi na kuhusika na biashara ya dawa za kulevya.

Alichezea sheria za uchaguzi. Hilo ndilo liliwakatisha tamaa wapinzani. Waligundua ingekuwa vigumu kushinda na kuchukua madaraka kwa njia ya uchaguzi mikononi mwa Maduro. Kilichofuata ni MUD kugawanyika, baadhi ya vyama vikageuka vikundi vya waasi na vingine vilifanya siasa kila kimoja kivyake.

Hali ikoje Malaysia

Ushindi wa muungano wa vyama vya Pakatan Harapan au Umoja wa Matumaini dhidi ya Barisan Nasional chini ya Waziri Mkuu, Najib Razak ulitokea kwa mshituko. Maana haukutarajiwa. Hata hivyo, aliyesababisha ni mwanasiasa mkongwe, Mahathir Mohamad.

Hakukuwa na matumaini yoyote kwa wapinzani kushika dola Malaysia, licha ya kwamba utawala uliopita chini ya Najib ulikuwa ukikabiliwa na kashfa nzito za rushwa, ukiukwaji wa haki za binadamu na utawala wa sheria. Ndipo Mahathir aliingia, naye akawapa sababu watu wa Malaysia kuwa mabadiliko yanawezekana.

Kitendo cha kufungwa jela mwasisi wa muungano wa Pakatan Harapan, Anwar Ibrahim mwaka 2015 kwa makosa ya kujihusisha na ‘usodoma’, kilifanya upinzani uonekane upo hohehahe katika kipindi ambacho kiu ya kumwondoa Najib madarakani ilikuwa kubwa kutokana na kashfa alizokuwa nazo.

Septemba 2016, Mahathir alijitenga na chama tawala cha UMNO ambacho kinaunda muungano wa Barisan Nasional, alichokuwa mwanachama wake tangu mwaka 1946 na kuanzisha chama cha Malaysian United Indigenous, kilichojiunga na muungano wa Pakatan Harapan.

Kitendo cha Mahathir kujiunga na Pakatan Harapan (PH) kisha kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa umoja huo, kuliwapa sababu wananchi wa Malaysia kupiga kura, maana waliona kwamba uwezekano wa Barisan Nasional (BN) kushindwa na kukabidhi madaraka ulikuwapo. Na matokeo yake, waliojitokeza kupiga kura walikuwa asilimia 82. PH wamepata viti vya ubunge 113 na BN 79.

Hali ya upinzani Tanzania

Kupitia kigezo cha tano katika nguzo za chama cha siasa, ni zamu ya kujiuliza kuhusu Tanzania na uelekeo wake wa kisiasa ikiwa imesalia miaka miwili kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu 2020. Je, wapinzani wameshawapa wananchi sababu ya kupiga kura?

Ikiwa uchaguzi mdogo wa wabunge majimbo ya Songea Mjini, Singida Kaskazini, Longido, Siha na Kinondoni yalifanyika na kuacha wapinzani wakiwalilia wananchi kuwa wamechezewa rafu, ni sababu ipi ambayo mwananchi anapewa kwamba katika Uchaguzi Mkuu 2020 apige kura na itahesabika kihalali?

Katika majimbo ya Songea Mjini, Singida Kaskazini na Longido, wapinzani – Ukawa na ACT-Wazalendo walisusa kabisa kwa hoja kuwa uchaguzi mdogo wa udiwani kata 43, uliofanyika Novemba mwaka jana ulijaa fujo, umwagaji damu na ubabe.

Kinondoni na Siha, Chadema na CUF (upande wa Profesa Ibrahim Lipumba) walishiriki, lakini CCM ilishinda majimbo hayo. Wakati CCM walipokuwa wanashangilia ushindi, wapinzani walikuwa wanalalamika kuibiwa kura na kufanyiwa rafu nyingi hasa siku yenyewe ya uchaguzi.

Msisitizo ni kuwa chama cha upinzani ili kujenga uungwaji mkono na kuwapa sababu wananchi watoke kwenda kukipigia kura, lazima pia kiwaaminishe kwamba chenyewe ni imara, kinaweza kusimamia vizuri hesabu ya kura zake na kikipata ushindi kitakabidhiwa dola.

Chama ambacho kinaonekana kipo lakini, kinajionyesha waziwazi kuwa hata kikishinda hakitakabidhiwa dola na hakutakuwa na tatizo lolote baada ya kukinyima kushika dola, japo kiwe kinapendwa sana kwa haiba ya viongozi wake au sera zake, bado hakiwezi kumfanya mwananchi akiwekee dhamana.

Hali ilivyo sasa nchini, ni wazi majaliwa ya Uchaguzi Mkuu 2020, ni ama CCM iendelee kushinda au ikataliwe na wananchi.

Hakuna upinzani imara. Uliopo unaparaganyika kama ilivyotokea Venezuela. Wapinzani hawaonyeshi kuwa na nguzo imara. Wanaishi kwa kutegemea kuhurumiwa kuliko mikakati ya kukua kuelekea kushika dola.

Kuna mawili kuelekea Uchaguzi Mkuu 2020. Ikitokea CCM ikishindwa basi wananchi watakuwa wameamua wenyewe. Ni kama ilivyotokea Gambia kwenye Uchaguzi wa Rais 2016, Adama Barrow wa Coalition 2016, hakushinda kwa nguvu ya upinzani, bali wananchi walimkataa aliyekuwa Rais, Yahya Jammeh.

Kabla ya uchaguzi, ilionekana Jammeh na chama chake cha Alliance for Patriotic Reorientation and Construction (APRC) wangeshinda, lakini wananchi kwa misingi ya ukabila walimkataa Jammeh.

Ni swali kwa wapinzani Tanzania; je, wanataka kushinda kwa uimara wa vyama vyao? Basi wafanye kazi sana. Kutegemea wananchi waamue kuikataa CCM, la sivyo itabidi wasubiri sana.

No comments