Kama Utakuwa Na Kitu Hiki, Kitakufanya Uwe Imara Na Mwenye Mafanikio Ya Kudumu
Fikiria kama kila kitu unachokihitaji wewe ingekuwa unakipata kila wakati hata pasipo kuweka juhudi kubwa, pasipo changamoto, pasipo kukipigania kitu hicho sana na wala pasipo hata kuweka kazi kubwa yoyote ile inayohitajika, ila kitu hicho unakipata.
Najua kama itatokea hivi, wengi wangefurahi sana na kusema hiyo itakuwa safi maana mambo yao yatakuwa yamewaendea sawa tena kwa uhakika. Lakini nikwambie ikitokea hivyo kwako ujue unakwenda kuwa dhaifu sana na mafanikio yako hayatadumu.
Nimekwambia utakwenda kuwa dhaifu na hautatengeneza mafanikio ya kudumu nikiwa na maana hii, changomoto yoyote itakayotokea hata kama ni ndogo kiasi gani hautaweza kukabilina nayo, kwa sababu mafanikio yako uliyapata kiulaini.
Mafanikio yoyote unayoyapata kwa njia rahisi sana pasipo kuyapigania uelewe hayana mizizi imara, hayana fundisho, hayana sehemu ambayo yamekukomaza na ndio maana huwezi kiuhalisia kukua kimafanikio bila kupambana kikamilifu.
Kama imetokea umepata mafanikio ya moja kwa moja pasipo kupitia changamoto, unatakiwa kuwa makini sana, la sivyo unaweza kupoteza kila kitu. Waangalie watu wanaopata bahati nasibu ni kitu gani kinawakuta baadae, wengi hufilisika tena.
Hiyo yote kama nilivyosema, inaonyesha huwezi kuwa na mafanikio imara na ya kudumu kama hujakutana na upinzani au changamoto za kutosha. Kila unapokutana na changamoto hizo hilo si swala la kuchukia bali ni kujifunza na kusonga mbele.
Maumivu unayokutana nayo wakati huu kwa sababu ya upinzani ama changamoto, wewe yavumilie kwani ni rafiki mkubwa sana wa mafanikio yako. Unaweza usione faida yake leo, lakini kesho utakuja kugundua kile nisemacho na kina ukweli gani.
Tambua kama hujawahi kushindwa, kama hujakosea, kama hujakutana na upinzani wa kutosha, halafu ukasema unataka mafanikio makubwa unajidanganya. Hata ukipata mafanikio yataporomoka kwa sababu hakuna kitu kilichokukomaza.
Majasiri na mashujaa katika maisha ni wale watu wote ambao wamepitia kwenye nyakati ngumu sana ambazo hata hazieleweki. Nyakati hizi ngumu ndizo ambazo zilizowajenga na kuwapa jeuri kubwa ya kuweza kufanikiwa.
Watu hawa ukiwaona wana nidhamu na ule uchungu wa maisha. Kuna kitu ambacho unaona kinachemka ndani mwao yaani wana kiu na hamasa kubwa sana ya kufanikiwa kwao. Yote hayo yanaletwa na upinzani ama changamoto walizokutana nazo.
Huhitaji kujilaumu, huhitaji kujuta kila unapokutana na changamoto kwani hapo ndipo nguvu kubwa ya mafanikio yako ya kudumu ilipo. Changamoto na upinzani mwingi unakuja kama rafiki wa kukusaidia kukukomaza na kukupa mafanikio ya kudumu.
Hata watu wengi katika maisha ni watu ambao hawapendi kusikia sana hadithi za watu ambao walifanikiwa moja kwa moja kwenye maisha. Hadithi za watu, ambao walifanikiwa moja kwa moja pasipo kupitia changamoto hazina mvuto.
Kila mtu anapenda sana kujifunza kwa watu ambao waliumia au watu ambao waliteseka juu ya changamoto fulani hivi, lakini mwisho wa siku wakaja kufanikiwa. Hivyo elewa, mafanikio ya moja kwa moja hayakupi nguvu na wala hayakukomazi .
Wewe hapo ulipo una nguvu kuliko unavyofikiri ya kukabiliana na changamoto yoyote ile. Ukiona umeshindwa wewe umeamua tu. Na changamoto yoyote unayokabiliana nayo ukiona umeishinda, tambua umepiga hatua fulani kubwa ya kimaisha.
Fanyia kazi haya na chukua hatua kuhakikisha ndoto zako zinatimia.
No comments